Na Mwondoshah Mfanga
Kwamba Raila Odinga wa ODM, mgombea urais Kenya ambaye anamlalamikia Rais Emilio Mwai Kibaki kwa kuiba kura ili kushinda katika kinyang`anyiro cha Urais mwezi uliopita, ataukwaa urais ni suala la siku au miezi michache tu na sio kwamba halipo au haliwezekani. Kila kigezo cha kisiasa na kisheria nchini Kenya na katika nyanja za kimataifa zinaonyesha kuwa kwa njia yoyote mambo yanavyokwenda yanaelekea kumweka Raila madarakani na Kibaki kuachia ngazi vinginevyo nchi itaingia katika mgogoro mkubwa zaidi wa kisiasa na kijamii. Kwa jinsi mambo yanavyokwenda nchini humo inaelekea kuwa Rais Kibaki hakuwa tayari kuachia madaraka baada ya kumaliza kipindi chake cha miaka mitato (2002-2007). Lakini pia inaelekea kwamba hakuwa pia amejitayarisha kuondoka baada ya kuona anaelekea kushindwa. Kinachotokea sasa ni kuwa, yaelekea Kibaki ameng`ang`ania kushika madaraka ili kujitayarisha kuondoka baada ya kuona kuwa ushindi wa Raila ni dhahiri. Dhana hapa zinapingana na inavyoelekea baadhi ya wanazuoni wa kisiasa wanautazama mgogoro uliopo Kenya kwa sasa kama vile ni suala tu la uchaguzi na kuibwa kwa kura mambo yalivyopelekea kutokea kwa maasi na mauaji. Wengine wanalitazama suala hili kama migongano ya kimakabila na hivyo wanaona kuwa kuondokana na hali hiyo pengine ni kugawanya majimbo mbalimbali ya nchi hiyo ili hatimaye kuua ule ushawishi wa makabila ambao unapelekea katika kusambaratisha umoja wa kitaifa. Lakini ukiitazama hali iliyopo nchini Kenya na historia yake tangu enzi za kupigania uhuru utaona kuwa mgogoro uliopo nchini humo sio suala la uchaguzi, wizi wa kura au ushindani katika misingi ya kikabila tu kama watu wengi wavyojaribu kubainisha mambo. Aliyekuwa Mshauri wa masuala ya kisiasa wa Rais Francois Miterand wa Ufaransa, Regis Debray, aliwahi kusema: Kamwe sisi binadamu hatupo makini katika kuzitazama zama zetu. Mara nyingi tunatazama historia katika jukwaa ikiwa imevaa baraka la wakati uliopita na tunapoteza maana ya mchezo mzima. Kila mara historia inaposonga mbele muendelezo katika kuiba dua na kuitalii ni lazima ufanywe, kwani wakati mwingine tunaweza tukaiona hali kuwa ni ya kawaida kumbe ni mapinduzi ya kweli.`` Hali ya Kenya na ile ya sasa ya Afrika ya Kusini, zinawatatanisha sana wanazuoni wengi, lakini zinaashiria kitu kimoja kikubwa kwamba kuna mapinduzi-fifi. Ile ya Kenya inaashiria kupatikana kwa kile baba wa Raila, Odinga Oginga, alichokiita ``Not yet Uhuru`` kwamba bado uhuru Kenya na bara la Afrika haujapatikana na kwamba hii inaashiria uhodhi wa madaraka ya kisiasa, ardhi na hata nyenzo za kiuchumi na baadhi ya watu au makabila yanayochukua nafasi ya Wakoloni. Hali inayojidhihirisha kikweli kweli ni ile ya walio nacho dhidi ya wale wasio nacho na kabila la Kikikuyu linaonekana kuwa limetumia nafasi liliyo nayo kwa ajili ya kuwaneemesha watu wake hata katika maeneo wanayoishi makabila mengine. Hii pia imelifanya kabila (ambalo pia lina watu wengi zaidi, ingawa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo kabla ya kuja kwa Kibaki, Daniel arap Moi aliwahi kusema kuwa hakuna kabila kubwa nchini humo kuliko lile la kwake la Wakalenjin) hili kushikilia madaraka ya kisiasa na pengine kuhakikisha kuwa yule anayeshika madaraka ya kisiasa ni lazima atimize matakwa ya kabila hilo ya kiuchumi. Lakini suala kubwa ni kuwa ni kwa nini baadhi ya wanasayansi wa siasa wanashikilia kuwa kinachotokea nchini Kenya sasa hivi ni mapinduzi ya Raila. Historia inatupeleka hadi nyuma wakati wa kupigania uhuru ambapo Wakenya wakishirikaina na chini ya Kenya African Union (KAU) na baadaye KANU walipata uhuru lakini mara tu baada ya uhuru huo baadhi ya viongozi wa juu nchini humo walitokea kuwatenga wanaharakati na kushikana na Wazungu katika harakati mpya za kuhakikisha kuwa Mkenya Mweusi anachukua nafasi ya Mkoloni Mweupe. Baba yake Raila anaandika katika kitabu chake cha `Not Yet uhuru` mara tu baada ya kutoka katika chama cha KANU na kuunda Kenya People Union (KPU) kuwa:``Ndani ya Kenya mapambano yaliyo mbele yetu sasa yatakuwa magumu ya nguvu na yenye kuhitaji uangalifu mkubwa. Tunapambana kuwazuia Wakenya Weusi wanaowasilisha matakwa ya watawala wa nchi hii kama warithi wa watawala walioondoka wa kikoloni… Sijidanganyi kwa kutoka kwangu ndani ya serikali hii iliyopo madarakani na kuunda chama kitakachotafuta ufumbuzi wa matatizo yanayowakabili wananchi wetu. Kwani adhima yetu ni kuwakilisha matakwa ya wananchi wa Kenya ambayo lazima yashinde hata kama harakati zenyewe zitakuwa za muda mrefu na ngumu.`` Oginga, Bildad Kaggia, Denis Akumu, Achieng Oneko, Tom Okelo-Odongo na baadhi ya wana KANU ni miongoni mwa wanachama wa chama hicho ambao waliachia ngazi na kuunda KPU mwaka 1966 wakieleza kuwa sera za serikali zilikuwa zinakwenda kinyume na makubaliano ya awali na kuwa walioshiriki katika kutafuta uhuru wa nchi hiyo walikuwa wamepanguliwa kando na badala yake wale wenye uhusiano na wakoloni ndio waliokalia madaraka. Oginga anatabiri kuwa mapinduzi ya Wakenya walio wengi na waliosahaulika yatakamilika hapo tu wengi kati ya wanaomaliza shule watapobaki bila kazi, wasio na kazi wanakuwa wakali katika mitaa na wasio na kazi, wenye kunyanyasika na wakulima watakapokufa njaa au kuingia katika hali ngumu ya kimaisha kiasi kwamba uvumilivu utashindikana. Ukitanzama hali ya Kenya kwa hivi sasa inaendana na utabiri huu uliofanywa zaidi ya miaka 40 iliyopita na baba mtu-wakati baadhi ya wakubwa wachache wa makabila fulani wakishirikana na Wazungu ndio wanaohodhi ardhi, wanaokufa njaa, maskini, wasio na kazi na jua kali, vibaka na wezi wanaongezeka mitaani na kuchafua amani na usalama wa nchi. Tatizo la Kenya ni kuwa mfumo wake wa uchumi na siasa unasadifu kabila moja au baadhi yenye nguvu za kiuchumi pia kutawala kisiasa na kuhodhi sehemu kubwa ya ardhi. Kwa hiyo mapinduzi ya Raila ambayo hayakuanza na muasisi huyu wa Orange Democratic Movement (ODM) bali baba yake hayakuanza jana. Katika chaguzi zote zilizopita hata wakati wa utawala wa Daniel arap Moi, mapambano siku zote yalikuwa ni katika vigezo hivi alivyokuwa akivipigania baba yake dhidi ya hodhi ya mali na wasio nacho. Tofauti ya wakati huu na nyakati zilizopita ni kuwa awali harakati hizi zilionekana kama ni vita ya Waluo dhidi ya Wakikuyu. Lakini jinsi siku zilivyokwenda inaelekea kama harakati za mapambano zimevuka vigezo hivi vya kikabila ambavyo vimekuwa vikitumika na hivyo masuala muhimu kuonekana kuwa ni walio nacho dhidi ya wasio nacho. Anazungumza mwandishi mmoja wa Kiingereza ambaye alikuwa nchini Kenya wakati wa uchaguzi kuwa suala sio tena la ukabila bali ni la wale walio nacho dhidi ya wale wasiokuwa nacho. Na kwa vile wengi walionacho wametokea kuwa ni Wakikuyu, basi inaonekana kama ni harakati baina ya makabila kumbe ukweli ni kuwa si hivyo. Jambo ambalo wapatanishi wanashindwa kuliona kwa sasa ni kuwa hali ya Kenya ni tete zaidi kuliko wanavyoiona na kwamba suala sio la uchaguzi ulioharibika peke yake. Bali ni kuwa ilibidi uchaguzi wenyewe uharibike au uharibiwe kutokana na hali ya utata uliyopo. Mahojiano na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Kenya Bw Kivuitu yanaonyesha kuwa, alikuwa anajua jambo fulani kubwa zaidi kati ya makundi ya wagombea hao wawili kabla hata ya kutangaza majibu na hivyo kuamua kuwa ni vema ampe ushindi Kibaki na sio Raila. Kwamba hata kama Raila ndiye aliyeshinda, angemtangaza haina maana kuwa kusingezuka fujo, na pengine kubwa zaidi kuliko zile zilizotokea kwa kutangazwa Kibaki. Hii ina maana kuwa alitoa maamuzi yake kwa kulingana na sosholojia pengine na saikolojia ya Wakenya zaidi kuliko kuangalia mshindi wa kweli. Hali ya kwamba wanaonyanyaswa wanataka kuchukua madaraka, lakini hawana dhima ya kufanya hivyo kwa sababu hali haiwaruhusu na hali ya kuwa walio na madaraka wanataka kuendelea kutawala lakini wanashindwa kufanya hivyo kwa sababu wakati wao umeshapita. Hizi ni alama za mapinduzi-fifi ambazo ni vema kuzielewa wakati wa kuchambua masuala ya kisiasa jamii yanayoitanza hali tete ya Kenya. Nini basi athari za mapinduzi-fifi haya. Moja ni kuwa endapo yatakamilika na Raila kushika madaraka hali ya Kenya itabadilika na kuwa kitu kingine kabisa ambacho, kinaweza pia kubadilisha hali nzima ya kisiasa na pengine uchumi katika eneo hili la Afrika. Suala la ukabila Kenya ni lazima litashughulikiwa, ikiwa ni pamoja na kugawa majimbo ya sasa ya nchi hiyo kuwa mengi zaidi kwa maana ya kujaribu kuondoa ukabila. Lakini mapinduzi makubwa zaidi ni yale yanayohusiana na tawala malimbali katika Afrika ambazo zimekuwa zikiiba kura katika kila uchaguzi ili kuendeleza kuwepo kwao katika madaraka. Kilichotokea Kenya kitakuwa ni somo kubwa sana na endapo Raila ataapishwa itapelekea watu wengi kujifunza kutokana na hali ya vurugu katika nchi hiyo. Tatu ni suala la ardhi ambalo limekuwa na ugumu wake katika nchi hiyo kwa maana ya kuwa sehemu kubwa ya nchi hiyo ilitoka katika mikono ya Wazungu na kuingia katika mikono ya Weusi wachache ambao ndio wanaoinyonya Kenya wakishirikiana na baadhi ya wakoloni. Hili litabadilika kwa kiwangoo kikubwa na pengine kuzifanya hali za Afrika ya Kusini, Namibia na Zimbabwe ambazo kwa kiasi fulani zinafanana nayo pia kubadilika. Jambo lingine ambalo pia litabadilika kwa kiwango kikubwa ni masuala yanayohusu wafanyakazi wa nchi hiyo na pengine katika nchi nyingine za Afrika ambapo aidha vyama vya wafanyakazi vilitekwa na vyama vya kifanyakazi vya kibeberu au na serikali zilizopo madarakani na kuwafanya wafanyakazi kupoteza haki zao na harakati katika kutafuta maslahi yao. Jumuiya ya Afrika Mashariki pia itabadilika na huenda suala la shirikisho likawa rahisi zaidi hususan ikitiliwa maanani kuwa, moja kati ya vigezo Watanzania walivyovitaja ni suala la ukabila Kenya, vita nchini Uganda na magomvi ya Watutsi na Wahutu huko Rwanda na Burundi.
SOURCE: Nipashe
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment