Tuesday, October 2, 2007

SERIKARI YA TANZANIA YAPANIA URAIA WA NCHI MBILI

Na Mobhare Matinyi, New York
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe, amesema serikali itahakikisha sheria ya uraia wa nchi mbili inapitishwa kwa manufaa ya Watanzania na taifa na si vinginevyo.Akizungumza na baadhi ya Watanzania waliokutana naye mjini New York(Mary Mitchell, Mobhare Matinyi,Namtasha Ikaweba, Shaaban Mseba, Augustino Malinda, Yasin Njayagha,Miraji Malewa,na Deogratias Rutabana) wiki iliyopita katika hoteli ya Grand Hyatt, Waziri Membe alisema lengo la serikali ni kuwasaidia Watanzania na si kugawa uraia wa Tanzania kwa wageni wenye uraia wa nchi zao.Alisema haingii akilini ni kwa nini Mtanzania wa kuzaliwa anyang’anywe uraia wa Tanzania kwa kuwa amechukua uraia wa nchi nyingine kutafuta faida za kielimu, ajira au hata matibabu.“Ni kwa nini tumuadhibu huyu Mtanzania wa kuzaliwa kwa kuwa tu amechukua uraia wa nchi nyingine ili apate elimu ama ajira na kusaidia ndugu zake waliobaki Tanzania?” alihoji Waziri Membe.Waziri alisisitiza kuwa sheria hiyo itakapopitishwa haitatoa mwanya kwa kila mtu kuuvamia uraia wa Tanzania bali itawalinda Watanzania wanaotaka kuchukua uraia wa nchi za nje kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.Akitoa mfano mmojawapo bila kutaja majina ya wahusika, Waziri Membe alisema anaifahamu familia moja ya Watanzania ambayo ililazimika kuchukua uraia wa Kanada kwa sababu za matibabu, na kwamba kuwanyang’anya uraia watu hawa ni kuwaadhibu bila kujali uhai wao.Alieleza kuwa familia hiyo ina watoto wawili ambao matibabu yao hugharimu dola 2,000 kwa kila mmoja kwa mwezi, na kwamba kwa kuchukua uraia wa Kanada, matibabu hayo yanakuwa bure. Alihoji je, ni haki kuwanyang’anya uraia wao wa Tanzania?Akitoa mfano wa manufaa yanayopatikana Ghana, Waziri Membe aliwaambia Watanzania hao kwamba ni muhimu kwa Tanzania kutumia raia wake walioko nje kwa manufaa ya taifa na siyo kuwabagua.“Mwaka jana pekee wananchi wa Ghana walioko nje waliingiza dola bilioni 2.5 kwa njia mbalimbali halali,” na akaongeza: “Taifa dogo kama Komoro, mwaka jana lilipata dola milioni 89 kutoka kwa wananchi wake walioko Ufaransa pekee.Akifafanua zaidi, Waziri Membe alisema wakati akiwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani kwa kipindi kisichofikia miaka miwili, Tanzania ilitoa uraia kwa wageni 101 na kushangaa ni kwa nini Watanzania wa kuzaliwa wapoteze uraia wao.Waziri Membe aliwataka Watanzania kujenga umoja thabiti na kuwahakikishia kwamba serikali itakuwa pamoja nao ili kuleta maendeleo kwa taifa, na kwamba mawazo kuwa usalama wa taifa utakuwa hatarini si la jambo kuhofia iwapo sheria itatungwa vizuri.Tanzania ina raia wake waliosambaa nchi mbalimbali duniani huku idadi kubwa ikiwa katika nchi za Kiarabu za Ghuba ambako wakati serikali ikiongeza ofisi moja ya Ubalozi nchini Oman miaka michache iliyopita ilikadiria kuwa kuna Watanzania laki tano.Nchi nyingine ambazo Watanzania wanakadiriwa kuwa wengi ni za Marekani Kaskazini na Ulaya Magharibi ambako wako kwa maelfu, ambao wengi wao hukabiliwa pia na utata wa uraia wa watoto wao wanaozaliwa ugenini.Mjadala wa suala la uraia wa nchi mbili umekuwa ukiendelea nchini katika siku za karibuni ambako kumeibuka kambi za wanaopinga kwa madai ya kulinda maslahi ya nchi na wanaounga mkono kwa madai hayo hayo ya kulinda maslahi ya nchi.

1 comment:

Anonymous said...

Hii ni sera safi sana. Watanzania tunaiunga mkono.

Bakashmar, Australia